![]() |
| Simba sport club |
Ikishuhudia timu ya Yanga wakichomoza na uongozi wa Ligi hiyo kwa kujikusanyia pointi…….. Nimekaa na kuiangalia Simba Sports Club kwenye misimu hii miwili, huu na ulioisha na kubaini wanapotea sana kwenye suala zima la usajili. Sitaki kuliingilia benchi lao la ufundi lililo chini ya kocha mwenye mafanikio na timu hiyo kwa muda wote mzee Abdallah ‘’King’’ Kibadeni, lakini Simba ya Mfaransa Patrick Liewing na Simba ya sasa ya Kibadeni hazina tofauti kubwa. Simba ya Liewing ilikosa mlinzi wa kati kwa ufasaha na mshambuliaji wa kusaidiana na Mzambia Felix Mumba Sunzu.
Huku Simba ya sasa ya mzee Kibadeni ikikosa kiungo mchezeshaji. Ni wachezaji wachache sana waliozaliwa kuwa viungo wachezeshaji. Mwinyi Kazimoto ni kiungo mchezeshaji wa mwisho kuichezea Simba kwa wakati huu.
Jonas Mkude, Abdullhalimu Humud, William Lucian,Henry Joseph na Saidi Ndemla hawa wote kiasili ni viungo wa kukaba, lakini cha kushangaza
zaidi unaweza kuona kwenye mchezo mmoja wakacheza wawili au watatu kati ya hao.
Huku wakiifanya timu ikabe zaidi kuliko kutengeneza mashambulizi kwa timu pinzani.
Saidi Ndemla ni miongoni mwa kiungo chipukizi anayekuja kwa kasi kubwa hapa nchini, hili ni zao la timu B ya Simba lililopandishwa timu kubwa, wakati yuko na timu B kocha wake Selemani Matola alikuwa akimtumia zaidi kwenye kiungo
cha kukaba, lakini sasa hivi Kibadeni anamtumia kwenye kiungo cha kushambulia, sasa hili ni tatizo kidogo maana akicheza kiungo cha kushambulia
mara nyingi husahau majukumu yake na kushuka chini kuja kukaba zaidi kuliko kuichezesha timu.
Kiukweli kwa sasa Simba haina kiungo wa kushambulia. Ina viungo wengi wa kukaba. Abdallah Sesseme ndiye kiungo anayeimudu kucheza nafasi ya kiungo
mshambuliaji, lakini kwenye mzunguko wote huu wa kwanza alikuwa majeruhi na wiki za hivi
karibuni ndiyo ameanza mazoezi mepesi mepesi. Viongozi na mashabiki wa Simba wanatakiwa kujua kwamba mpira ni zaidi ya kucheza.
Mpira unahitaji nidhamu ya nje ya uwanja na ndani mwa uwanja ndipo mchezaji atafanikiwa
kwenye malengo yake ya uchezaji.
Ramadhani Chombo ni miongoni mwa viungo bora kabisa kwenye ukanda huu wa Afrika mashariki, lakini nidhamu yake iko chini mno.
Nakumbuka msimu uliyoisha alikuwemo kwenye kundi la wachezaji waliosimamishwa kwa utovu wa nidhamu na kocha wa kipindi hiko Patrick Liewing.
Kabla ya kuanza kwa msimu huu aliufata uongozi wake na kuuomba radhi kwa vitendo vyake hivyo.
Uongozi ukamsamehe na kurudishwa tena kwenye timu, lakini cha kushangaza karudia zaidi karudia tena utovu wake wa nidhamu na muda mwingi kwenye mzunguko wa kwanza aliutumia timu B kuliko timu kubwa.
Sanjari na hilo mashabiki wanatakiwa kujua hakuna kocha yeyote Duniani anaependa kupanga kikosi dhaifu ili timu yake ifungwe, ila hupanga kikosi chake kwa kuangalia vitu vingi ikiwemo nidhamu ya mchezaji na hali ya mchezaji kiujumla.
Nimeitizama Simba kwenye michezo yake ya mwisho mwisho mwa mzunguko wa kwanza na
kubaini kila inapocheza mchezo wa Ligi kuu morali yao, hali yao ya ushindi na mashabiki kuzidi kupungua, huku mpinzani wake mkubwa Yanga wakizidi kuimalika siku hadi siku.
Nahisi Simba ya msimu huu imefanya usajili bila ya kupitia ripoti yake msimu uliyoisha.
Imesajili wachezaji wanaofanana kwa sifa zote uwanjani Zahoro Pazi na Sinno Augustino.
Hawa nao wanaingia kwenye kundi hili, Girlbert Kaze Demunga na Joseph Owino ni miongoni mwa walinzi bora kabisa kwenye ukanda huu wa Afrika mashariki na kati, lakini nao pia wanafanana kwa kila kitu uwanjani, huwa wanatumia akili zaidi kuliko nguvu ni nzuri lakini Simba inatakiwa isajili beki wa kati mwingine mwenye matumizi ya nguvu
na akili.
Mwishoni mwa mwezi uliopita nilikuwa namsikiliza kwenye chombo kimoja cha habari hapa nchini kocha Kibadeni akihojiwa kuhusu hali za wachezaji wake. Akatamka hadharani baadhi
ya mambo yanayofanyika kwenye kambi yao ya Bamba Beach nje kidogo ya jiji la Dar-es-
salam, hiki kilikuwa si kitendo kizuri hata kidogo kwa kocha mwenye uzoefu kama Kibadeni
kutokeza mbele ya hadhira na kuongelea mambo yanayofanywa na wachezaji wake, huku akamalizia kwa kusema mshambuliaji Edward Christopher ameshuka kiwango, wakati hata mchezo mmoja wa Ligi kuu alikuwa hajacheza, sasa hiko kiwango cha Cristopher kimeshuka mazoezini..?
Nilitegemea angekuja na kuwatetea wachezaji mbele ya waandishi na kuwaambia jinsi kambi yao inavyoendelea vizuri.
Nimekuwa mfuatiliaji mzuri wa kocha Kibadeni, amekuwa na tabia ya kutoa visingizio vya hapa na pale pindi timu yake ikiwa haifanyi vizuri.
Huku akisahau kama Simba ni miongoni mwa timu zilizoanza maandalizi ya Ligi kuu mapema sana.
Kuna utamaduni umeibuka Simba msimu huu, kwa mzunguko wa kwanza mchezaji akicheza
chini ya kiwango hata kwa mechi 1 hupelekwa timu B ili aboreshe kiwango chake.
Ni nzuri sana ila ina mapungufu. Haroun Chanongo na Abdullhalim ni miongoni mwa viungo
walioisaidia sana timu mpaka kufikia hapa ilipo lakini imetokea sintofahamu kwa wachezaji hawa mpaka wameshushwa timu ya B.
Inaaminika kilichosababisha kushushwa kwao kwenye timu B ni kuonekana wamecheza chini ya kiwango kwenye mchezo dhidi ya Yanga.
Hiki si kitendo cha kiungwana hata kidogo. Kucheza chini ya kiwango kwa mchezaji ni suala la kawaida.
Simba ilitakiwa kuwaacha kwenye timu kubwa wafanye mazoezi kama kawaida na wenzao
mpaka hapo watakaporudi kwenye fomu zao za kawaida ndipo waanze tena kwenye kikosi chao cha kwanza.
Lakini kuwapeleka timu B ni kuwabomoa zaidi na siyo kuboresha kiwango. Henry Joseph naye aliingia kwenye kundi hili la kupelekwa timu B kwa kupishana kauli na makocha wake.
Hapa ndipo panaponisikitisha zaidi timu B iko kwa mchezaji anayeshuka kiwango, lakini Henry alipelekwa huko kwa sababu alipishana kauli na makocha wake.
Nilitegemea makocha wauambie uongozi kuhusu suala hili la Henry ili achukuliwe hatua za kisheria kama kukatwa mshahara na posho zake lakini siyo kupelekwa timu B.
‘’Simba wanatakiwa wayaangalie haya ya msingi
ili kujenga amani na ushikamano’’
HUU NI MTAZAMO WANGU
AGE-22
ABDULLY MKEYENGE- 0718 32 24 49

No comments:
Post a Comment